Kuanzia saa za asubuhi za Jumapili hii, tarehe 17 Mei 2026, shughuli za kuvuka mipaka inayounganisha Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika Wilaya ya Rubavu zimesimamishwa kwa muda, ikiwa ni hatua ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Ebola unaoendelea kusambaa kwa kasi nchini DRC.
Hatua hiyo imekuja wakati taasisi za afya duniani zinaendelea kutoa tahadhari kuhusu ongezeko la maambukizi na vifo vinavyosababishwa na Ebola katika Mkoa wa Ituri nchini DRC, ambapo tayari watu wengi wanaripotiwa kushukiwa kuambukizwa huku vifo kadhaa vikithibitishwa.
Shirika la Afya Duniani, World Health Organization pamoja na Africa Centres for Disease Control and Prevention, vimeonya kuwa mlipuko huo una hatari ya kusambaa katika nchi jirani za DRC kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu na hali ya usalama isiyo imara mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zinaonyesha kuwa Rwanda imeimarisha hatua za ukaguzi kwa watu wanaoingia na kutoka mipakani, kwa lengo la kuzuia ugonjwa wa Ebola kuingia nchini humo.
Bagabo John
