Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameweka hadharani ratiba rasmi ya ziara ya nyota wa zamani wa klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya England, Rio Ferdinand, baada ya kuwasili nchini Tanzania kwa ziara maalum ya michezo na utalii.
Akizungumza mara baada ya ujio wa nyota huyo maarufu, Makonda alisema kuwa ujio wa Ferdinand ni sehemu ya juhudi za kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia michezo, utamaduni na vivutio vya utalii. Alieleza kuwa Ferdinand atatembelea maeneo mbalimbali muhimu pamoja na kushiriki shughuli kadhaa za kijamii na michezo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, Ferdinand anatarajiwa kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo hifadhi za taifa, kukutana na wadau wa michezo nchini pamoja na kushiriki matukio maalum yatakayowakutanisha mashabiki wa soka na vijana wanaochipukia katika mchezo huo.

Makonda amesema kuwa ziara hiyo inalenga kuendelea kuitangaza Tanzania duniani kupitia watu maarufu wenye ushawishi mkubwa katika michezo. Aidha, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki matukio mbalimbali yatakayomhusisha Ferdinand wakati wote wa ziara yake nchini.


Rio Ferdinand anatajwa kuwa mmoja wa mabeki bora kuwahi kutokea katika soka la England, ambapo aliwahi kupata mafanikio makubwa akiwa na Manchester United ikiwemo kutwaa mataji mbalimbali ya Ligi Kuu England pamoja na mashindano ya Ulaya.
Bagabo John
