Janet Kagame amefungua Imbuto Hub, kituo kilichopo wilayani Bugesera, ambacho kimejengwa kwa ushirikiano kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Bugesera na Imbuto Foundation. Kituo hicho kinalenga kuwawezesha vijana kwa kuwapatia fursa za kujifunza, kukuza ubunifu na ujuzi, pamoja na kutoa huduma zitakazonufaisha wananchi kwa ujumla.
Imbuto Hub ni kituo kilichoanzishwa kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupitia ubunifu, michezo, elimu, burudani na mafunzo ya ufundi.
Pia kinatoa huduma za ushauri wa afya na ustawi wa jamii, pamoja na malezi ya watoto, huku kikitarajiwa kunufaisha wananchi wote wa eneo husika.
Kituo hiki kina vyumba 20 vinavyoruhusu shughuli mbalimbali kufanyika kwa wakati mmoja. Vinajumuisha ukumbi wa mazoezi ya viungo, viwanja vya michezo, maktaba, kituo cha watoto, madarasa ya ufundi, mafunzo ya urembo, Karate na kituo cha teknolojia.
Aidha, Imbuto Hub huwahudumia pia wazee kwa kuwapa mazoezi ya viungo ya jioni yanayowasaidia kudumisha afya, kupunguza upweke na kuimarisha mahusiano ya kijamii. Katika miezi mitatu ya kwanza, kituo hicho kilikuwa kikipokea wastani wa vijana 200 kwa siku na kuwahudumia maelfu ya wananchi kupitia huduma zake mbalimbali.
Imbuto Hub ni mradi wa Imbuto Foundation ulioanzia Bugesera, na unatarajiwa kupanuliwa katika wilaya zote za Rwanda ili kuwapa vijana fursa zaidi za michezo, mafunzo ya ufundi na matumizi ya teknolojia.
Bagabo John
