Mwamuzi wa mpira wa miguu wa Somalia, Omar Abdulkadir Artan, amekuwa gumzo duniani baada ya kuzuiwa kuingia nchini Marekani alipokuwa akielekea kushiriki Kombe la Dunia la FIFA 2026 kama mwamuzi rasmi.
Tukio hilo limezua mjadala mkubwa, hasa kutokana na ukweli kwamba Artan alikuwa ameandikwa historia kama Msomali wa kwanza kuteuliwa kuchezesha mechi za Kombe la Dunia.
Artan, ambaye alitajwa kuwa Mwamuzi Bora wa Afrika mwaka 2025, alikuwa tayari amepata visa ya Marekani na alikuwa miongoni mwa waamuzi 52 walioteuliwa na FIFA kwa mashindano hayo.
Hata hivyo, alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Miami, maafisa wa uhamiaji wa Marekani walimzuia kuingia nchini humo wakidai kulikuwa na kile walichokiita "masuala ya uchunguzi wa kiusalama" (vetting concerns).

Serikali ya Marekani baadaye ilisema iliona sababu zilizomfanya asiweze kuruhusiwa kuingia nchini, ingawa maelezo kamili hayakuwekwa hadharani.
Artan mwenyewe amekanusha kuhusika na makundi yoyote ya kigaidi.
Baada ya kurejea nyumbani mjini Mogadishu, Artan alipokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi, viongozi wa michezo na mashabiki wa soka.
Mamia ya watu walikusanyika kumpokea kama shujaa wa taifa, wakisema kwamba licha ya kukosa nafasi ya kuchezesha Kombe la Dunia, mafanikio yake ya kufika kiwango hicho tayari yalikuwa ushindi mkubwa kwa Somalia.
Picha na video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha umati wa watu ukimshangilia na kumkaribisha kwa heshima kubwa.
Akizungumza baada ya kurejea nyumbani, Artan alisema kuwa kilichotokea anakiona kama "majaliwa" (fate) na akawahimiza Wasomali kutokata tamaa.
Alisisitiza kuwa ataendelea kuitumikia Somalia na kwamba tukio hilo halitabadilisha upendo wake kwa taifa lake. Kauli hiyo iliwagusa wengi na kuongeza zaidi heshima aliyonayo miongoni mwa wananchi wa Somalia.

Ingawa Omar Artan alikosa fursa ya kuweka historia katika Kombe la Dunia 2026 kutokana na kuzuiwa kuingia Marekani, nchini Somalia ameonekana kama shujaa aliyefungua milango kwa kizazi kipya cha waamuzi na wanamichezo wa taifa hilo.
Bagabo John
